Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 9

9
Kuteuliwa kwa Israeli na Mwenyezi Mungu
1Ninasema kweli katika Al-Masihi, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho wa Mungu. 2Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu. 3Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Al-Masihi kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili, 4yaani watu wa Israeli. Hao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea Torati, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi. 5Wao ni wa uzao wa baba zetu wa zamani, ambao kutoka kwao Al-Masihi alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen.
6Si kwamba neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi. 7Wala hawawi wazao wa Ibrahimu kwa sababu wao ni watoto wake, lakini: “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaka.”#9:7 Mwanzo 21:12 8Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Ibrahimu. 9Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”#9:9 Mwanzo 18:10, 14
10Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani baba yetu Isaka. 11Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lolote jema au baya, ili kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama, 12si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”#9:12 Mwanzo 25:23 13Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau.”#9:13 Malaki 1:2, 3
Mwenyezi Mungu hana upendeleo
14Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha! 15Kwa maana Mungu alimwambia Musa,
“Nitamrehemu yeye nimrehemuye,
na pia nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”#9:15 Kutoka 33:19
16Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu. 17Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili hasa, ili nipate kuonesha uweza wangu juu yako, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani kote.”#9:17 Kutoka 9:16
18Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.
19Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?” 20Lakini, ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’#9:20 Isaya 29:16; 45:921Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?
22Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu? 23Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake? 24Hivi vyombo ni sisi, ambao pia alituita, sio kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu wa Mataifa.
Yote yalitabiriwa katika Maandiko
25Kama alivyosema Mungu katika Hosea:
“Nitawaita ‘watu wangu’#9:25 Hosea 2:23
wale ambao si watu wangu;
nami nitamwita ‘mpendwa wangu’
yeye ambaye si mpendwa wangu,”
26tena,
“Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa,
‘Ninyi si watu wangu,’#9:26 Hosea 1:10
wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ”
27Isaya anapaza sauti na kusema kuhusu Israeli kwamba:
“Ingawa idadi ya Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani,
ni mabaki yao tu watakaookolewa.
28Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitekeleza
hukumu yake duniani kwa haraka
na kwa ukamilifu.”#9:28 Isaya 10:22, 23
29Ni kama vile alivyotabiri Isaya, akisema:
“Kama Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
hakutuachia uzao,
tungekuwa kama Sodoma,
tungefanana na Gomora.”#9:29 Isaya 1:9
Kutokuamini kwa Israeli
30Kwa hiyo tuseme nini? Kwamba watu wa Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kupitia kwa imani. 31Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kupitia kwa sheria, hawakuipata. 32Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kupitia kwa imani bali kupitia kwa matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza”. 33Kama ilivyoandikwa:
“Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza watu
na mwamba wa kuwaangusha.
Yeyote atakayemwamini
hataaibika kamwe.”#9:33 Isaya 8:14; 28:16

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia