Warumi 15:22-33
Warumi 15:22-33 NENO
Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu. Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi hadi huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. Ila sasa niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walio miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Al-Masihi. Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi na kwa upendo wa Roho wa Mungu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu. Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walio Yudea, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu, ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.