Warumi 15:22-33
Warumi 15:22-33 SRUV
Ndiyo sababu nilizuiwa mara nyingi nisije kwenu. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kuja kwenu; wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana natarajia kuwaona ninyi nikiwa katika safari, na kusafirishwa nanyi, baada ya kukaa kwenu kwa muda. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumia watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kutoa mchango kwa ajili ya watakatifu walio maskini huko Yerusalemu. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumia kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia mhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo. Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe kutoka kwa wale wasioamini katika Yudea, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.