Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Warumi 16

16
Salamu kwa watu binafsi
1Napenda kumtambulisha kwenu dada yetu Foibe, mhudumu katika kundi la waumini la Kenkrea. 2Naomba mpokeeni katika Bwana Isa ipasavyo watakatifu na kumpa msaada wowote atakaohitaji kutoka kwenu, kwa maana yeye amekuwa msaada kwa watu wengi, mimi nikiwa miongoni mwao.
3Wasalimuni Prisila#16:3 kwa Kiyunani ni Priska na Akila, watumishi wenzangu katika Al-Masihi Isa. 4Wao walihatarisha maisha yao kwa ajili yangu; wala si mimi tu ninayewashukuru bali pia makundi yote ya waumini walio watu wa Mataifa.
5Salimuni pia kundi la waumini wanaokutana nyumbani mwao.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto, aliyekuwa mtu wa kwanza kumwamini Al-Masihi huko jimbo la Asia.
6Msalimuni Mariamu, aliyefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu.
7Wasalimuni Androniko na Yunia, jamaa zangu ambao wamekuwa gerezani pamoja nami. Wao ni maarufu miongoni mwa mitume, nao walikuwa katika Al-Masihi kabla yangu.
8Msalimuni Ampliato, yeye nimpendaye katika Bwana Isa.
9Msalimuni Urbano, mtendakazi mwenzetu katika Al-Masihi, pamoja na rafiki yangu mpendwa Stakisi.
10Msalimuni Apele aliyejaribiwa na akaithibitisha imani yake katika Al-Masihi.
Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Aristobulo.
11Msalimuni ndugu yangu Herodioni.
Wasalimuni wote walio nyumbani mwa Narkiso walio katika Bwana Isa.
12Wasalimuni Trifaina na Trifosa, wale wanawake wanaofanya kazi kwa bidii katika Bwana Isa.
Msalimuni rafiki yangu mpendwa Persisi, mwanamke mwingine aliyefanya kazi kwa bidii katika Bwana Isa.
13Msalimuni Rufo, mteule katika Bwana Isa, pamoja na mama yake, ambaye amekuwa mama kwangu pia.
14Wasalimuni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herma na ndugu wote walio pamoja nao.
15Wasalimuni Filologo, Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa na watakatifu wote walio pamoja nao.
16Salimianeni kwa busu takatifu.
Makundi yote ya waumini ya Al-Masihi wanawasalimu.
Maelekezo ya mwisho
17Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana wetu Al-Masihi, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga. 19Kila mtu amesikia kuhusu utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.
20Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.
Neema ya Bwana wetu Isa iwe nanyi. Amen.
21Timotheo, mtendakazi mwenzangu anawasalimu. Vivyo hivyo Lukio, Yasoni, na Sosipatro, ndugu zangu.
22Mimi, Tertio, niliye mwandishi wa waraka huu, nawasalimu katika Bwana Isa.
23Gayo, ambaye ni mwenyeji wangu na wa kundi lote la waumini, anawasalimu.
Erasto, mweka hazina wa mji huu, pamoja na Kwarto ndugu yetu, pia wanawasalimu.
[ 24Neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi iwe pamoja nanyi nyote. Amen.]#16:24 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.
Maneno ya mwisho ya kumsifu Mwenyezi Mungu
25Sasa atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara kwa Injili yangu na kuhubiriwa kwa Isa Al-Masihi, kutokana na kufunuliwa siri zilizofichika tangu zamani za kale. 26Lakini sasa siri hiyo imefunuliwa na kujulikana kupitia maandiko ya kinabii kutokana na amri ya Mungu wa milele, ili mataifa yote yaweze kumwamini na kumtii: 27ndiye Mungu, aliye pekee mwenye hekima, ambaye kupitia kwa Isa Al-Masihi utukufu ni wake milele na milele! Amen.

Iliyochaguliwa sasa

Warumi 16: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia