Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho Utangulizi

Utangulizi
Korintho ulikuwa mji uliojengwa pwani ya Mediterania (yaani Bahari Kuu). Mji huu ulistawi kwani ulikuwa kituo kikuu cha biashara. Ulikuwa koloni la Kirumi, ukiwavutia wakazi wa mataifa mbalimbali, wakiwemo Warumi, Wayunani na Wayahudi kutoka sehemu zilizoizunguka Bahari Kuu. Mchanganyiko huu wa wakazi ulisababisha kuharibika na kuzorota kwa maadili.
Paulo alianzisha kundi la waumini wa Isa mjini Korintho katika safari yake ya pili kueneza Injili, na akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Aliondoka Korintho akifuatana na Prisila na Akila kwenda Efeso, na kutoka huko alitembelea kundi la waumini la Yerusalemu, na baadaye akarudi Antiokia. Paulo alipokea habari kutoka kwa nyumba ya Kloe kwamba kundi la waumini lilikuwa limegawanyika. Paulo aliona ni muhimu awaandikie waraka huu ili kujibu matatizo mengi yaliyojitokeza. Aliposhughulikia matatizo haya moja kwa moja, Paulo alifafanua misingi ya mafundisho ya wafuasi wa Al-Masihi kuhusu imani na maadili.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Kusudi
Kusahihisha makosa dhahiri katika kundi la waumini wa Isa huko Korintho, na pia kuwaelimisha waumini jinsi ya kumtumikia Al-Masihi katika jamii iliyokosa maadili.
Mahali
Efeso.
Tarehe
Mnamo 55 B.K.
Wahusika Wakuu
Paulo, Timotheo, nyumba ya Kloe, waumini wa Korintho.
Wazo Kuu
Umuhimu wa mwenendo wa mfuasi wa Al-Masihi kufanana na Al-Masihi.
Mambo Muhimu
Suluhu za matatizo mbalimbali kama: ugomvi katika kundi la waumini, uzinzi, kushtakiana, mabishano juu ya ndoa, chakula kilichotolewa kwa sanamu, hali ya Paulo kuwa mtume, matumizi mabaya ya Chakula cha Bwana Isa, ukweli kuhusu ufufuo, na mengine. Lazima mwenendo wa mfuasi wa Al-Masihi ufanane na ule wa Al-Masihi; kukosa kufanya hivyo ni kumwaibisha Al-Masihi na jumuiya ya waumini wake.
Yaliyomo
Salamu za Paulo (1:1-9)
Tatizo la mgawanyiko katika kundi la waumini (1:10–4:21)
Tatizo la zinaa katika kundi la waumini (5:1-13)
Tatizo la kushtakiana mahakamani (6:1-11)
Tatizo la uasherati (6:12-20)
Tatizo kuhusu ndoa (7:1-40)
Matatizo kuhusu uhuru binafsi (8:1–11:16)
Matatizo kuhusu Chakula cha Bwana Isa na ibada (11:17–14:40)
Matatizo kuhusu ufufuo wa wafu (15:1-58)
Mawaidha ya mwisho (16:1-24).

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia