Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 1

1
Salamu
1Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Al-Masihi Isa, na Sosthene ndugu yetu.
2Kwa kundi la waumini wa Mungu walioko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Al-Masihi Isa na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Al-Masihi Isa Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia.
3Neema na amani zinazotoka kwa Mungu, Baba#1:3 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yetu, na kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi ziwe nanyi.
Shukrani
4Ninamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu kwa sababu ya neema yake mliyopewa katika Al-Masihi Isa. 5Kwa kuwa katika Al-Masihi mmetajirishwa kwa kila hali, katika kusema kwenu na katika maarifa yenu yote, 6kwa sababu ushuhuda wetu kumhusu Al-Masihi ulithibitishwa ndani yenu. 7Kwa hiyo hamkupungukiwa na karama yoyote ya kiroho wakati mnangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa Bwana wetu Isa Al-Masihi. 8Atawafanya imara hadi mwisho, ili msiwe na hatia siku ile ya Bwana wetu Isa Al-Masihi. 9Mungu ambaye mmeitwa naye ili mwe na ushirika na Mwanawe Isa Al-Masihi, Bwana wetu ni mwaminifu.
Mgawanyiko katika kundi la waumini
10Nawasihi ndugu zangu, katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi, kwamba mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi, ili pasiwepo na matengano kati yenu, na kwamba mwe na umoja kikamilifu katika nia na katika kusudi. 11Ndugu zangu, nimepata habari kutoka kwa baadhi ya watu wa nyumbani mwa Kloe kwamba kuna magomvi kati yenu. 12Maana yangu ni kwamba: Mmoja wenu husema, “Mimi ni wa Paulo”; mwingine, “Mimi ni wa Apolo”; mwingine, “Mimi ni wa Kefa#1:12 yaani Petro”; na mwingine, “Mimi ni wa Al-Masihi.”
13Je, Al-Masihi amegawanyika? Je, Paulo ndiye alisulubishwa kwa ajili yenu? Je, mlibatizwa#1:13 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao. kwa jina la Paulo? 14Nashukuru kwamba sikumbatiza mtu yeyote isipokuwa Krispo na Gayo. 15Kwa hiyo hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba alibatizwa kwa jina langu. 16(Naam, niliwabatiza pia watu wa nyumbani mwa Stefana; lakini zaidi ya hao sijui kama nilimbatiza mtu mwingine yeyote.) 17Kwa maana Al-Masihi hakunituma ili kubatiza bali kuhubiri Injili; sio kwa maneno ya hekima ya kibinadamu, ili msalaba wa Al-Masihi usije ukakosa nguvu yake.
Al-Masihi ni hekima na nguvu ya Mwenyezi Mungu
18Kwa maana ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. 19Kwa maana imeandikwa:
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima,
na kubatilisha akili ya wenye akili.”#1:19 Isaya 29:14
20Yuko wapi mwenye hekima? Yuko wapi msomi? Yuko wapi mwanafalsafa wa nyakati hizi? Je, Mungu hakufanya hekima ya ulimwengu huu kuwa upumbavu? 21Kwa kuwa katika hekima ya Mungu ulimwengu kwa hekima yake haukumjua yeye, ilimpendeza Mungu kuwaokoa walioamini kwa upuzi wa lile neno lililohubiriwa. 22Wayahudi wanadai ishara za miujiza na Wayunani wanatafuta hekima. 23Lakini sisi tunamhubiri Al-Masihi aliyesulubiwa: yeye kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni upuzi. 24Lakini kwa wale ambao Mungu amewaita, Wayahudi na pia Wayunani, Al-Masihi ndiye nguvu ya Mungu na pia hekima ya Mungu. 25Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.
26Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika vyeo. 27Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima; Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Al-Masihi Isa, aliyefanyika kwetu hekima inayotoka kwa Mungu, yaani haki yetu, na utakatifu na ukombozi. 31Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Mwenyezi Mungu.”#1:31 Yeremia 9:24

Iliyochaguliwa sasa

1 Wakorintho 1: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia