1 Wakorintho 2
2
Kumtangaza Al-Masihi aliyesulubiwa
1Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu chochote nilipokuwa nanyi, isipokuwa Isa Al-Masihi aliyesulubiwa. 3Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya ushawishi, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho wa Mungu, 5ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.
Hekima ya kweli itokayo kwa Mwenyezi Mungu
6Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuumbwa, kwa ajili ya utukufu wetu. 8Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati hizi aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangeelewa, hawangemsulubisha Bwana wa utukufu. 9Lakini ni kama ilivyoandikwa:
“Hakuna jicho limepata kuona,
wala sikio limepata kusikia,
wala hayakuingia moyoni mwa mwanadamu yeyote,
mambo ambayo Mungu amewaandalia
wale wanaompenda”#2:9 Isaya 64:4:
10Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa Roho wake.
Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu. 11Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho Mtakatifu wa Mungu. 12Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13Haya ndio tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa maneno ya kiroho. 14Mtu ambaye hana Roho hawezi kupokea mambo yanayotoka kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa upambanuzi wa rohoni. 15Mtu wa kiroho hubainisha mambo yote, lakini yeye mwenyewe habainishwi na mtu yeyote.
16“Kwa maana ni nani aliyefahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu
ili apate kumfundisha?”#2:16 Isaya 40:13
Lakini sisi tunayo mawazo ya Al-Masihi.
Iliyochaguliwa sasa
1 Wakorintho 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.