Ruthu 1
1
Naomi na Ruthu
1Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi. Mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda, pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu. 2Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu, wakaishi huko.
3Elimeleki mumewe Naomi akafa, hivyo Naomi akabaki na wanawe wawili. 4Nao wakaoa wanawake Wamoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya kuishi huko miaka kumi, 5Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.
6Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba Mwenyezi Mungu amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakwe wake wakajiandaa kurudi nyumbani. 7Yeye na wakwe wake wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.
8Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe wake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani mwa mama yake. Mwenyezi Mungu na awatendee mema kama mlivyowatendea hao waliofariki, na mimi pia. 9Mwenyezi Mungu na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani mwa mume mwingine.”
Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa, 10wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe kwa watu wako.”
11Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi? 12Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, 13je, mngesubiri hadi wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa Mwenyezi Mungu umekuwa kinyume nami!”
14Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.
15Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
16Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakoenda nami nitaenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Mwenyezi Mungu na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
19Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”
20Akawaambia, “Msiniite tena Naomi#1:20 maana yake Kupendeza, Kufurahisha; niiteni Mara#1:20 maana yake Chungu, kwa sababu Mwenyezi#1:20 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania pia ms 21. amenitendea mambo machungu sana. 21Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini Mwenyezi Mungu amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? Mwenyezi Mungu amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”
22Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabu mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.
Iliyochaguliwa sasa
Ruthu 1: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.