2 Kor 7:8-16
2 Kor 7:8-16 SUV
Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu. Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote. Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo. Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu. Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lo lote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli. Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka. Nafurahi, kwa sababu katika kila neno nina moyo mkuu kwa ajili yenu.