Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Sam 18:9-18

2 Sam 18:9-18 SUV

Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni. Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi. Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu. Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga. Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni. Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua. Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia watu. Nao wakamtwaa Absalomu wakamtupa katika shimo kubwa mle msituni, wakaweka juu yake chungu kubwa sana la mawe; kisha Israeli wote wakakimbia kila mtu hemani mwake. Huyo Absalomu alipokuwa yu hai alikuwa ameitwaa na kujiinulia ile nguzo iliyoko bondeni mwa mfalme; kwa maana alisema, Mimi sina mtoto wa kulikumbusha jina langu; akaiita hiyo nguzo kwa jina lake mwenyewe nayo inaitwa ziara la Absalomu hata hivi leo.