Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Sam 23:8-23

2 Sam 23:8-23 SUV

Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, mkuu wa maakida; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja. Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao; huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti; ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai. Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu. Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango! Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA. Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu. Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu. Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theluji; huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe. Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu. Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamweka juu ya walinzi wake.