2 Samueli 23:8-23
2 Samueli 23:8-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Yafuatayo ni majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi: Yosheb-bashebethi, Mtakmoni, aliyekuwa kiongozi wa wale watatu, yeye alipigana kwa mkuki wake, akaua watu 800 wakati mmoja. Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, wa ukoo wa Mwahohi. Siku moja, Eleazari alikuwa pamoja na Daudi walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika kupigana vita. Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. Lakini Eleazari alisimama imara na kupigana na Wafilisti mpaka mkono wake uliposhindwa kupinda, ukabaki umeshikilia upanga wake. Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Baada ya ushindi huo, Waisraeli walirudi mahali alipokuwa Eleazari na kujipatia nyara za bure kutoka kwa Wafilisti waliouawa. Shujaa wa tatu alikuwa Shama mwana wa Agee, Mharari. Wafilisti walikusanyika huko Lehi, mahali palipokuwa na shamba la dengu nyingi, nao Waisraeli waliwakimbia Wafilisti. Lakini alisimama imara katikati ya shamba hilo ili kulitetea, naye akawaua Wafilisti. Mwenyezi-Mungu alijipatia ushindi mkubwa. Kisha, mashujaa watatu kati ya wakuu thelathini waliteremka wakati wa mavuno wakamfikia Daudi kwenye pango huko Adulamu. Wakati huo jeshi la Wafilisti lilikuwa limepiga kambi katika bonde la Refaimu. Naye Daudi wakati huo alikuwa katika ngome, nalo jeshi la Wafilisti lilikuwa mjini Bethlehemu. Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango la mji!” Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi alikataa kuyanywa, na badala yake, akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu, akisema, “Kamwe, sina haki ya kunywa maji haya, ee Mwenyezi-Mungu; je, haya si kama damu ya wale walioyahatarisha maisha yao kuyaleta maji haya?” Kwa hiyo, Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndiyo mambo waliyotenda wale mashujaa watatu. Abishai nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Je, huyo hakuwa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa watatu? Kwa hiyo akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu. Naye Benaya mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa theluji, alishuka shimoni na kuua simba. Vilevile, aliliua jitu la Misri. Mmisri huyo alikuwa na mkuki, lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumwua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe. Benaya, mwana wa Yehoyada alifanya mambo haya, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu. Basi, akawa mashuhuri kati ya wale mashujaa thelathini, ingawa hakuwa kama wale mashujaa watatu. Na Daudi akampa cheo cha mkuu wa walinzi wake binafsi.
2 Samueli 23:8-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, Hamkuu wa wakuu wa majeshi; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja. Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao; huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo shamba lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti; ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai. Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu. Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango! Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilichokuwa karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; lakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA. Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatarisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu. Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu. Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa kamanda wao; ila hakuweza kuwa kama wale watatu. Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wawili wakali wa Moabu, pia aliingia katika shimo na kumwua simba wakati wa theluji; huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyang'anya Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe. Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu. Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamteua kuwa mkuu wa walinzi wake.
2 Samueli 23:8-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, mkuu wa maakida; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja. Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao; huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti; ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai. Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu. Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango! Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA. Akasema, Hasha, BWANA, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu. Tena, Abishai, nduguye Yoabu, mwana wa Seruya, alikuwa mkuu wa wale watatu. Huyo aliuinua mkuki wake juu ya watu mia tatu, akawaua, akawa na jina kati ya wale watatu. Je! Huyo hakuwa na heshima maalumu miongoni mwa wale watatu? Kwa hiyo akawekwa kuwa akida wao; ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Tena Benaya, mwana wa Yehoyada, mtu hodari wa Kabseeli aliyekuwa amefanya mambo makuu; aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theluji; huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe. Hayo ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, akawa na jina kati ya wale mashujaa watatu. Alikuwa mwenye heshima kuliko wale thelathini, ila hakudiriki kuwamo katika wale watatu. Naye Daudi akamweka juu ya walinzi wake.
2 Samueli 23:8-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi: Yosheb-Bashebethi Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia nane, aliowaua katika pambano moja. Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai Mwahohi. Akiwa mmoja wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha Waisraeli wakarudi nyuma, lakini yeye alisimama imara, akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na kugandamana na upanga. Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari kuteka tu nyara za waliokufa. Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia. Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalipigania na kuwaua Wafilisti, naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa. Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya wale mashujaa thelathini wakuu walimwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai. Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!” Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Mwenyezi Mungu, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walienda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa. Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu. Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. Je, hakupata heshima kubwa kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao. Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe. Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.