Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 23:8-23

2 Samweli 23:8-23 NENO

Haya ndiyo majina ya mashujaa wa Daudi: Yosheb-Bashebethi Mtahkemoni, alikuwa kiongozi wa wale Watatu; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia nane, aliowaua katika pambano moja. Wa pili wake alikuwa Eleazari mwana wa Dodai Mwahohi. Akiwa mmoja wa wale mashujaa watatu, alikuwa pamoja na Daudi wakati waliwadhihaki Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko Pas-Damimu kwa ajili ya vita. Kisha Waisraeli wakarudi nyuma, lakini yeye alisimama imara, akawaua Wafilisti hadi mkono wake ukachoka na kugandamana na upanga. Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa siku ile. Vikosi vikarudi kwa Eleazari kuteka tu nyara za waliokufa. Aliyefuata alikuwa Shama mwana wa Agee Mharari. Wafilisti walipokusanyika pamoja mahali palipokuwa shamba lililojaa dengu, vikosi vya Israeli viliwakimbia. Lakini Shama akasimama imara katikati ya lile shamba. Akalipigania na kuwaua Wafilisti, naye Mwenyezi Mungu akawapa ushindi mkubwa. Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya wale mashujaa thelathini wakuu walimwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai. Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!” Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Mwenyezi Mungu. Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Mwenyezi Mungu, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walienda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa. Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu. Abishai ndugu yake Yoabu mwana wa Seruya ndiye alikuwa kiongozi wa hao Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu mia tatu ambao aliwaua, kwa hiyo naye akawa na sifa kama hao Watatu. Je, hakupata heshima kubwa kuliko hao Watatu? Alikuwa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao. Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli ambaye alifanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua mashujaa wawili waliokuwa hodari kuliko wote wa Moabu. Pia alishuka shimoni kulipokuwa na theluji na kumuua simba. Pia alimuua Mmisri mrefu mkubwa. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki mkononi mwake, Benaya alimwendea akiwa na rungu. Alipokonya mkuki kutoka mkononi mwa Mmisri na kumuua kwa mkuki wake mwenyewe. Haya yalikuwa mambo ya ushujaa ya Benaya mwana wa Yehoyada; naye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu. Daudi akamweka kuwa kiongozi wa walinzi wake.