Mdo 25:1-12
Mdo 25:1-12 SUV
Hata Festo alipokwisha kuingia katika uliwali, baada ya siku tatu akapanda kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria. Kuhani Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi, na kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea na kumwua njiani. Lakini Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yu tayari kwenda huko karibu. Akasema, Wale walio na mamlaka kwenu na watelemke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko neno baya katika mtu huyu. Alipokwisha kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akatelemkia Kaisaria; hata siku ya pili akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe. Alipokuja, wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu yake wakaleta mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha. Paulo akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya hekalu, wala juu ya Kaisari. Lakini Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo? Paulo akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana. Basi ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka rufani kwa Kaisari. Basi Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.