Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Eze 47:1-12

Eze 47:1-12 SUV

Baadaye akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Tena itakuwa, wavuvi watasimama karibu nao; toka Engedi mpaka En-eglaimu, patakuwa ni mahali pa kutandazia nyavu; samaki wao watakuwa namna zao mbalimbali, kama samaki wa bahari kubwa, wengi sana. Bali mahali penye matope, na maziwa yake, hayataponywa; yataachwa yawe ya chumvi. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.