Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 47:1-12

Ezekieli 47:1-12 BHN

Yule mtu akanirudisha kwenye kiingilio cha hekalu. Huko, maji yalikuwa yakitoka chini ya kizingiti cha hekalu kuelekea upande wa mashariki, (kwa maana hekalu lilielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitiririka kutoka chini ya upande wa kusini wa lango la hekalu, kusini mwa madhabahu. Kisha akanipeleka nje kwa njia ya lango la kaskazini. Akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, upande wa mashariki; na maji yalikuwa yanatoka upande wa kusini. Yule mtu, kwa ufito wake wa kupimia, akapima mita 500 kwenda chini upande wa mashariki, akanipitisha kwenye maji. Maji yalifika kwenye nyayo tu. Kisha akapima tena mita 500, akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka magoti yangu. Akapima tena mita nyingine 500, naye akaniongoza kuvuka maji. Maji yakafika mpaka kiunoni mwangu. Akapima mita 500 nyingine, na mto ukawa na kilindi kirefu hata sikuweza kuuvuka tena. Haikuwezekana kuuvuka ila kwa kuogelea. Yule mtu akaniambia, “Wewe mtu! Zingatia mambo hayo yote kwa makini.” Kisha, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Nilipofika huko niliona miti mingi sana kwenye kingo za mto. Akaniambia, “Maji haya yanatiririka kupitia nchini hadi Araba; na yakifika huko yatayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji mazuri. Kila mahali mto huu utakapopita, kutaishi aina zote za wanyama na samaki. Mto huu utayafanya maji ya Bahari ya Chumvi kuwa maji baridi. Kokote utakakopita utaleta uhai. Wavuvi watasimama ufuoni mwa bahari, na eneo kutoka Engedi mpaka En-eglaimu litakuwa la kuanikia nyavu zao. Kutakuwa na aina nyingi za samaki kama zilivyo katika Bahari ya Mediteranea. Lakini sehemu zake zenye majimaji na mabwawa kando ya bahari, hazitakuwa na maji mazuri. Bali hayo yatabaki kuwa maji ya chumvi. Kisha ukingoni mwa mto huo kutaota kila namna ya miti itoayo chakula. Majani yake hayatanyauka wala miti hiyo haitaacha kuzaa matunda. Itazaa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu inapata maji yanayotiririka kutoka maskani ya Mungu. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatatumika kuponya magonjwa.”