Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yn 9:24-41

Yn 9:24-41 SUV

Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi. Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona. Basi wakamwambia, Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani? Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake? Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako. Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho! Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo. Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote. Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje. Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye. Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia. Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu? Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.