Yohane 9:24-41
Yohane 9:24-41 BHN
Basi, wakamwita tena huyo aliyekuwa kipofu, wakamwambia, “Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi.” Yeye akajibu, “Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona.” Basi, wakamwuliza, “Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?” Huyo mtu akawajibu, “Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, nyinyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?” Lakini wao wakamtukana wakisema, “Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose. Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!” Naye akawajibu, “Hili ni jambo la kushangaza! Nyinyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu! Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake. Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!” Wao wakamjibu, “Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?” Basi, wakamfukuza sunagogini. Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuza sunagogini. Basi, alipomkuta akamwuliza, “Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?” Huyo mtu akajibu, “Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini.” Yesu akamwambia, “Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa.” Basi, huyo mtu akasema, “Ninaamini Bwana!” Akamsujudia. Yesu akasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, “Je, sisi pia ni vipofu?” Yesu akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa nyinyi mwasema: ‘Sisi tunaona,’ na hiyo yaonesha kwamba mna hatia bado.