Omb 2:1-12
Omb 2:1-12 SUV
Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni Kwa wingu katika hasira yake! Ameutupa toka mbinguni hata nchi Huo uzuri wa Israeli; Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake Katika siku ya hasira yake. Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme na wakuu wake. Ameikata pembe yote ya Israeli Katika hasira yake kali; Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume Mbele ya hao adui, Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao, Ulao pande zote. Ameupinda upinde wake kama adui, Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi; Naye amewaua hao wote Waliopendeza macho; Katika hema ya binti Sayuni Amemimina kani yake kama moto. Bwana amekuwa mfano wa adui, Amemmeza Israeli; Ameyameza majumba yake yote, Ameziharibu ngome zake; Tena amemzidishia binti Yuda Matanga na maombolezo. Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu, Kana kwamba ni ya bustani tu; Ameziharibu sikukuu zake; BWANA amezisahauzisha katika Sayuni Sikukuu za makini na sabato; Naye amewadharau mfalme na kuhani Katika uchungu wa hasira yake. Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA Kama katika siku ya kusanyiko la makini. BWANA amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika. Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa BWANA. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.