Mt 28:8-15
Mt 28:8-15 SUV
Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.