Mathayo 28:8-15
Mathayo 28:8-15 NENO
Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, lakini wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. Ghafula, Isa akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. Ndipo Isa akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kupanga njama, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha, wakawaambia, “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” Hivyo basi, wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi hadi leo.