Zab 35:1-10
Zab 35:1-10 SUV
Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.