Zab 78:1-8
Zab 78:1-8 SUV
Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu, Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu. Na nifunue kinywa changu kwa mithali, Niyatamke mafumbo ya kale. Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu, Ambayo baba zetu walituambia. Hayo hatutawaficha wana wao, Huku tukiwaambia kizazi kingine, Sifa za BWANA, na nguvu zake, Na mambo yake ya ajabu aliyoyafanya. Maana alikaza ushuhuda katika Yakobo, Na sheria aliiweka katika Israeli. Aliyowaamuru baba zetu Wawajulishe wana wao, Ili kizazi kingine wawe na habari, Ndio hao wana watakaozaliwa. Wasimame na kuwaambia wana wao Wamwekee Mungu tumaini lao. Wala wasiyasahau matendo ya Mungu, Bali wazishike amri zake. Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu.