Zab 78:40-55
Zab 78:40-55 SUV
Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani. Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng’ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.