Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 22:41-53

1 Wafalme 22:41-53 SRUV

Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi. Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa BWANA. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu. Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli. Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Yuda? Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi. Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme. Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; lakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi. Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali. Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake. Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli. Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake.