1 Wafalme 22:41-53
1 Wafalme 22:41-53 BHN
Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Ahabu wa Israeli, Yehoshafati mwana wa Asa, alianza kutawala Yuda. Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba binti Shilhi. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya baba yake Asa. Lakini hakupaharibu mahali pa kutambikia vilimani. Watu waliendelea kutambikia na kufukiza ubani mahali hapo. Yehoshafati pia, alifanya mapatano ya amani na mfalme wa Israeli. Matendo mengine ya Yehoshafati, ushujaa wake na vita alivyopigana, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda. Wafiraji wote wa kidini waliosalia tangu nyakati za baba yake Asa, Yehoshafati aliwaondoa nchini. Katika nchi ya Edomu, hapakuwa na mfalme. Nchi hiyo ilitawaliwa na naibu. Mfalme Yehoshafati aliunda meli za kwenda Ofiri kuleta dhahabu lakini hazikufika kwa sababu zilivunjikavunjika huko Esion-geberi. Basi, Ahazia mwana wa Ahabu, akamwambia Yehoshafati, “Waache watumishi wangu wasafiri pamoja na watumishi wako katika meli.” Lakini Yehoshafati hakukubali jambo hilo. Hatimaye, Yehoshafati alifariki, na kuzikwa pamoja na babu zake katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi baba yake; naye Yehoramu, mwanawe, akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda, Ahazia, mwana wa Ahabu, alianza kutawala Israeli. Alitawala kwa muda wa miaka miwili, kutoka Samaria. Ahazia alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; aliuiga mwenendo wa baba yake na mwenendo wa Yezebeli, mama yake, na wa Yeroboamu, mwana wa Nebati ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Alimtumikia na kumwabudu Baali, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kila jambo kama alivyofanya baba yake.