1 Wafalme 22:41-53
1 Wafalme 22:41-53 NENO
Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na tano. Mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi. Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakuenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoshafati, mafanikio aliyokuwa nayo na uhodari wake katika vita, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa. Wakati ule, hakukuwa na mfalme katika Edomu; naibu ndiye alitawala. Wakati huu Yehoshafati akaunda merikebu nyingi za biashara ili kwenda Ofiri kuchukua dhahabu; lakini kamwe hazikusafiri, kwa maana zilivunjikia huko Esion-Geberi. Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa. Kisha Yehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika mji wa Daudi baba yake. Yehoramu mwanawe akawa mfalme baada yake. Ahazia mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda. Naye akatawala katika Israeli kwa miaka miwili. Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa sababu alienenda katika njia za baba yake na mama yake na katika njia za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye alisababisha Israeli itende dhambi. Alimtumikia na kumwabudu Baali na kumghadhibisha Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.