Ezekieli 7:1-13
Ezekieli 7:1-13 SRUV
Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Na wewe, mwanadamu, Bwana MUNGU aiambia hivi nchi ya Israeli; Ni mwisho; mwisho umezijia pembe nne za nchi. Sasa mwisho huu unakupata, nami nitakuletea hasira yangu, nitakuhukumu kulingana na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitakuachilia, wala sitaona huruma; bali nitakupatiliza njia zako, na machukizo yako yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, jambo baya la namna ya peke yake; angalia, linakuja. Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja. Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani. Basi hivi karibu nitamwaga ghadhabu yangu juu yako, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga. Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka. Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao. Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata watu wote. Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu watu wote; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.