Mwanzo 43:24-34
Mwanzo 43:24-34 SRUV
Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakanawa miguu, akawapa punda wao chakula. Wakaiweka tayari ile zawadi hadi atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka chini. Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? Wakasema, Mtumishi wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu. Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mama yake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu. Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulilia, akaingia chumbani mwake, akalilia humo. Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula. Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri. Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa haki ya uzawa wake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao. Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafurahi pamoja naye.