Mwanzo 43:24-34
Mwanzo 43:24-34 NENO
Msimamizi akawapeleka wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji ya kunawa miguu, na kuwapa punda wao majani. Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yusufu atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko. Yusufu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia. Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama, wakamsujudia. Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.” Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yusufu akaondoka kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo. Baada ya kunawa uso wake, akarudi; huku akijizuia kulia, akasema, “Pakueni chakula.” Wakampakulia Yusufu peke yake, nao ndugu zake peke yao, na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri. Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao. Walipopelekewa sehemu ya chakula kutoka meza ya Yusufu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.