Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 2:2-13

Hosea 2:2-13 SRUV

Msihini mama yenu, msihini; kwa maana yeye si mke wangu, wala mimi si mume wake; na aondokane na usherati wake usiwe mbele ya uso wake, na uzinzi wake usiwe kati ya matiti yake; nisije nikamvua nguo zake akawa uchi, nikamweka katika hali aliyokuwa nayo siku ya kuzaliwa kwake, na kumfanya kama jangwa, na kumweka kama nchi kame, na kumwua kwa kiu; naam, sitawaonea rehema watoto wake; kwa maana ni watoto wa uzinzi. Maana mama yao amezini; yeye aliyewachukua mimba ametenda mambo ya aibu; maana alisema, Nitafuatana na wapenzi wangu, wanipao chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na vileo vyangu. Basi kwa ajili ya hayo, angalia, nitaiziba njia yako kwa miiba, nami nitafanya kitalu juu yake, asipate kuyaona mapito yake. Naye atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; atawatafuta, lakini hatawaona; ndipo atakaposema, Nitakwenda nikamrudie mume wangu wa kwanza; kwa maana hali yangu ya zamani ilikuwa njema kuliko hali yangu ya sasa. Maana hakujua ya kuwa mimi ndiye niliyempa ngano, na divai, na mafuta, na kumwongezea fedha na dhahabu, walivyovitumia kwa ajili ya Baali. Basi kwa ajili ya hayo, nitaitwaa tena ngano yangu kwa wakati wake, na divai yangu kwa wakati wake, nami nitamnyang'anya sufu yangu na kitani yangu, vya kumfunika uchi wake. Na sasa nitaifunua aibu yake mbele ya macho ya wapenzi wake, wala hapana mtu atakayemwokoa katika mkono wangu. Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamriwa. Nami nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema, Hii ndiyo ujira wangu niliopewa na wapenzi wangu; nami nitaifanya kuwa msitu, na wanyama wa mashamba wataila. Nami nitamwadhibu kwa sababu ya siku za Mabaali, aliowafukizia uvumba; hapo alipojipamba kwa pete masikioni mwake, na kwa vito asema BWANA.

Soma Hosea 2