Hosea 2:2-13
Hosea 2:2-13 BHN
Mlaumuni mama yenu mlaumuni, maana sasa yeye si mke wangu wala mimi si mume wake. Mlaumuni aondokane na uasherati wake, ajiepushe na uzinzi wake. La sivyo, nitamvua nguo abaki uchi, nitamfanya awe kama alivyozaliwa. Nitamfanya awe kama jangwa, nitamweka akauke kama nchi kavu. Nitamuua kwa kiu. Na watoto wake sitawahurumia, maana ni watoto wa uzinzi. Mama yao amefanya uzinzi, aliyewachukua mimba amefanya mambo ya aibu. Alisema; “Nitaambatana na wapenzi wangu, ambao hunipa chakula na maji, sufu na kitani, mafuta na divai.” Basi, nitaiziba njia yake kwa miiba, nitamzungushia ukuta, asipate njia ya kutokea nje. Atawafuata wapenzi wake, lakini hatawapata; naam, atawatafuta, lakini hatawaona. Hapo ndipo atakaposema, “Nitarudi kwa mume wangu wa kwanza; maana hapo kwanza nilikuwa nafuu kuliko sasa.” Hakujua kwamba ni mimi niliyempa nafaka, divai na mafuta, niliyemjalia fedha na dhahabu kwa wingi, ambazo alimpelekea Baali. Kwa hiyo wakati wa mavuno nitaichukua nafaka yangu, nitaiondoa divai yangu wakati wake. Nitamnyang'anya nguo zangu za sufu na kitani, ambazo zilitumika kuufunika uchi wake. Nitamvua abaki uchi mbele ya wapenzi wake, wala hakuna mtu atakayeweza kunizuia. Nitazikomesha starehe zake zote, sikukuu zake za mwezi mwandamo na za Sabato, na sikukuu zote zilizoamriwa. Nitaiharibu mizabibu yake na mitini, anayosema ni malipo kutoka kwa wapenzi wake. Nitaifanya iwe misitu, nao wanyama wa porini wataila. Nitamlipiza sikukuu za Baali alizoadhimisha, muda alioutumia kuwafukizia ubani, akajipamba kwa pete zake na johari, na kuwaendea wapenzi wake, akanisahau mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema.