Yakobo 2:14-26
Yakobo 2:14-26 SRUV
Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mmoja wenu akawaambia, Nendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya kimwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? Je! Baba yetu Abrahamu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Abrahamu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.