Yakobo 2:14-26
Yakobo 2:14-26 NENO
Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, naye mmoja wenu akamwambia, “Nenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? Vivyo hivyo, imani peke yake, kama haikuambatana na matendo, imekufa. Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.” Nioneshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo. Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani wanaamini hivyo na kutetemeka. Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? Je, Ibrahimu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni? Unaona jinsi imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. Kwa njia hiyo likatimizwa andiko lisemalo, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu. Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake. Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba: je, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? Kama vile mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.