Waamuzi 5
5
Wimbo wa Debora
1Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;
2Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli,
Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao,
Mhimidini BWANA.
3Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu;
Mimi, naam mimi, nitamwimbia BWANA;
Nitamhimidi BWANA, Mungu wa Israeli.
4 #
Kum 33:2; Zab 68:7,8; Hab 3:3-6; Isa 64:3 BWANA, ulipotoka katika Seiri,
Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu,
Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondosha maji,
Naam, mawingu yakadondosha maji.
5 #
Kut 19:18; Kum 4:11 Milima ikayeyuka mbele za uso wa BWANA,
Naam hata Sinai ule mbele za uso wa BWANA, Mungu wa Israeli.
6 #
Amu 3:31; Law 26:22; Isa 33:8; Omb 1:4; 4:18 Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi,
Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu;
Nayo misafara ilipita kwa njia za kando.
7 #
Amu 4:4-6; Isa 49:23 Watawala walikoma katika Israeli, walikoma,
Hadi mimi Debora nilipoinuka,
Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.
8 #
Kum 32:16; Amu 2:12; 1 Sam 13:19,22; Amu 4:3 Walichagua miungu mipya,
Ndipo kulikuwa na vita malangoni;
Je! Ilionekana ngao au mkuki
Katika watu elfu arubaini wa Israeli?
9Moyo wangu unawaelekea makamanda wa Israeli,
Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu;
Mhimidini BWANA.
10 #
Amu 12:14
Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe,
Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani,
Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.
11Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji,
Hapo watatangaza matendo ya haki ya BWANA;
Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli.
Ndipo watu wa BWANA waliposhuka malangoni.
12Amka, amka, Debora;
Amka, amka, imba wimbo.
Inuka, Baraka, wachukue mateka wao
Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.
13Ndipo waliteremka mabaki ya waungwana na ya watu;
BWANA alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.
14 #
Amu 3:27; 4:5,6; Hes 32:39; Mwa 49:21 Kutoka Efraimu waliteremka wao ambao shina lao ni katika Amaleki,
Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako.
Kutoka Makiri walishuka makamanda,
Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.
15Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora.
Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka.
Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake.
Kwenye vijito vya Reubeni
Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
16 #
Hes 32:1
Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo,
Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi?
Kwenye vijito vya Reubeni
Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
17 #
Yos 13:25; 19:29 Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani,
Na Dani, mbona alikaa katika merikebu?
Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari,
Alikaa katika hori zake.
18 #
Amu 4:10
Zabuloni ndio watu waliohatarisha roho zao hadi kufa;
Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.
19 #
Amu 4:16; Zab 44:12 Wafalme walikuja wakafanya vita,
Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita.
Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido;
Hawakupata faida yoyote ya fedha.
20 #
Yos 10:11; Amu 4:15 Walipigana kutoka mbinguni,
Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.
21 #
Amu 4:7
Mto ule wa Kishoni uliwachukua,
Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni.
Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.
22Kisha, kwa kishindo kwato za farasi zilipigapiga,
Kwa maana walivyoenda shoti,
Walipowakimbiza farasi wenye nguvu.
23 #
Amu 21:9; Neh 3:5; 1 Sam 17:47 Ulaanini Merozi, alisema malaika wa BWANA,
Walaanini kwa uchungu wenyeji wake;
Kwa maana hawakuja kumsaidia BWANA,
Kumsaidia BWANA juu ya hao wenye nguvu.
24 #
Mit 31:31; Lk 1:28 Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote;
Mkewe Heberi, Mkeni,
Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.
25Aliomba maji, naye akampa maziwa.
Akamletea siagi katika sahani ya heshima.
26Akanyosha mkono wake akashika kigingi,
Nao mkono wake wa kulia ukashika nyundo ya fundi;
Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake.
Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.
27Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala.
Miguuni pake aliinama, akaanguka.
Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.
28Alichungulia dirishani, akalia,
Mama yake Sisera alilia dirishani;
Mbona gari lake linakawia kufika?
Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?
29Mabibi wake wenye akili wakamjibu,
Naam, alijipa jawabu.
30 #
Kut 15:9
Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya,
Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu?
Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbalimbali,
Nyara za mavazi ya rangi mbalimbali ya darizi;
Ya rangi mbalimbali ya darizi, pande zote mbili,
Juu ya shingo za hao mateka.
31 #
Zab 48:4,5; 58:11; Ufu 6:10; 18:20; 2 Sam 23:4; Zab 37:6; Mt 13:43; Zab 19:5 Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee BWANA.
Bali wao wampendao na wawe kama jua hapo litokapo kwa nguvu zake. Nayo nchi ikastarehe miaka arubaini.
Iliyochaguliwa sasa
Waamuzi 5: SRUV
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.