Yohana 13:1-17
Yohana 13:1-17 SRUV
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, huku akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye akiwa amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, moyo wa kumsaliti; Yesu, huku akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Akamfikia Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe waniosha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutaniosha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Nisipokuosha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga mwili hana haja ila ya kuosha miguu, maana yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwaosha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha miguu, imewapasa ninyi pia kuoshana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo. Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyemtuma. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.