Yohana 15:18-27
Yohana 15:18-27 SRUV
Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi niliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenituma. Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana kisingizio kwa dhambi yao. Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure. Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.