Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 3:45-66

Maombolezo 3:45-66 SRUV

Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa. Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao. Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. Jicho langu lachuruzika mito ya machozi Kwa sababu ya kuharibiwa kwa binti zangu. Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; Hata BWANA atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa ajili ya kuangamizwa kwa binti wa watu wangu. Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. Nililiitia jina lako, BWANA, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. Ee BWANA umenitetea katika kisa cha nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu. Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee BWANA; Unihukumie neno langu. Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu. Ee BWANA, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu; Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa. Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi. Utawalipa malipo, Ee BWANA, Sawasawa na kazi ya mikono yao. Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao. Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za BWANA.