Luka 16:19-31
Luka 16:19-31 SRUV
Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa walikuwa wakija na kumramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Abrahamu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Abrahamu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Abrahamu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, aupoze ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Abrahamu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo yako mema katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unateseka. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Abrahamu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Abrahamu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishika hata mtu akifufuka katika wafu.