Mathayo 28:8-15
Mathayo 28:8-15 SRUV
Wakaondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; nendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya walinzi waliingia mjini, wakawaambia wakuu wa makuhani juu ya mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na jambo hili likisikika kwa mtawala, sisi tutasema naye, nanyi hamtapata shida. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.