Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 22:1-31

Zaburi 22:1-31 SRUV

Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Lakini Wewe U Mtakatifu, Utukuzwaye na sifa za Israeli. Baba zetu walikutumainia Wewe, Walitumainia, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumainia, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Nimedharauliwa na kupuuzwa na watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee BWANA; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinisalimisha matitini mwa mama yangu. Kwako nilitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi. Mafahali wengi wamenizunguka, Walio hodari wa Bashani wamenisonga; Wananifumbulia vinywa vyao, Kama simba apapuraye na kunguruma. Nimemwagika kama maji, Mifupa yangu yote imeteguka, Moyo wangu umekuwa kama nta, Na kuyeyuka ndani ya moyo wangu. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; Unaniweka katika mavumbi ya mauti Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; Wamenidunga mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote; Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, BWANA, usiwe mbali, Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia. Uniponye nafsi yangu na upanga, Mpenzi wangu na nguvu za mbwa. Kinywani mwa simba uniokoe; Naam, toka pembe za nyati umenijibu. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, Katikati ya kusanyiko nitakusifu. Ninyi mnaomcha BWANA, msifuni, Enyi nyote mlio wazawa wa Yakobo, mtukuzeni, Mcheni, enyi nyote mlio wazawa wa Israeli. Maana hapuuzi Wala kuchukizwa na mateso ya anayeteswa, Wala hamfichi uso wake, Bali humsikia akimlilia. Kwako zinatoka sifa zangu Katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu Mbele yao wamchao. Wapole watakula na kushiba, Wamtafutao BWANA watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele. Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea BWANA; Jamaa zote za mataifa watamsujudia. Maana ufalme ni wa BWANA, Naye ndiye awatawalaye mataifa. Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, Humwinamia wote washukao mavumbini; Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake, Wazawa wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za BWANA, Kwa kizazi kitakachokuja, Watautangaza wokovu wake kwa watakaozaliwa, Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.

Soma Zaburi 22