Zaburi 35:19-28
Zaburi 35:19-28 SRUV
Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e. Maana hawasemi maneno ya amani, Ila juu ya watulivu wa nchi huwaza hila. Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona. Wewe, BWANA, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami. Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu. Unihukumu kwa haki yako, Ee BWANA, Mungu wangu, Na usiwaache wanisimange. Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza. Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu. Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe BWANA, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake. Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.