Zaburi 37:16-26
Zaburi 37:16-26 SRUV
Kidogo alicho nacho mwenye haki ni bora Kuliko wingi wa mali wa wasio haki wengi. Maana mikono ya wasio haki itavunjika, Bali BWANA huwategemeza wenye haki. BWANA huwatunza waaminifu, Na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, Na siku za njaa watashiba. Bali wasio haki watapotea, Nao wamchukiao BWANA watatoweka, Kama uzuri wa mashamba, Kama moshi watatoweka. Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. Maana waliobarikiwa na BWANA watairithi nchi, Nao waliolaaniwa naye watakatiliwa mbali. Hatua za mtu mwema huimarishwa na BWANA, Naye huipenda njia yake. Ajapojikwaa hataanguka chini, Maana BWANA humshika mkono na kumtegemeza. Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzawa wake akiomba chakula. Mchana kutwa hufadhili na kukopesha, Na mzao wake hubarikiwa.