Zaburi 45:1-8
Zaburi 45:1-8 SRUV
Moyo wangu umefurika kwa jambo jema, Mimi nasema niliyomfanyia mfalme; Ulimi wangu ni kama kalamu ya mwandishi stadi. Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele. Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako. Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli, upole na haki Na mkono wako wa kulia Utakutendea mambo ya ajabu. Mishale yako ni mikali, katika mioyo ya adui za mfalme; Watu huanguka chini yako. Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako. Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.