Ufunuo 16:8-16
Ufunuo 16:8-16 SRUV
Na huyo wa nne akalimimina bakuli lake juu ya jua, nalo likaruhusiwa kuwaunguza wanadamu kwa moto. Wanadamu wakaunguzwa na joto kali, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. Na huyo wa tano akalimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. Na huyo wa sita akalimimina bakuli lake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha lile joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. (Tazama, naja kama mwizi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) Wakawakusanya hadi mahali paitwapo kwa Kiebrania, Harmagedoni.