Ufunuo 20:1-6
Ufunuo 20:1-6 SRUV
Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa na ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia mhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe kwa muda mfupi. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa mamlaka ya kutoa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala kuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliobakia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.