Mwanzo 25
25
Wazawa wengine wa Abrahamu#25:1-6 Si ajabu kwamba katika simulizi hili Abrahamu anaonekana kuwa babu wa makundi kadha wa kadha ya mataifa Ya Kiarabu na pia Wamidiani. Ingawa si rahisi kutambulisha mataifa hayo kwa uhakika, yahusu mataifa yaliyotawanyika huku na huko katika eneo la Kusini-Mashariki ya nchi ya Kanaani na kufikia Arabia.
(1 Nya 1:32-33)
1Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura. 2Ketura alimzalia Abrahamu: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. 3Yokshani alimzaa Sheba na Dedani; wazawa wa Dedani walikuwa Waashuru, Waletushi na Waleumi. 4Watoto wa Midiani#25:4 Wana wa Midiani: Hawa wanatajwa mara kadhaa katika A.K. (rejea Kut 2:16; 3:1; 18:1; Zab 83:9; Isa 9:4). walikuwa Efa, Eferi, Henoki, Abida na Eldaa. Wote hao walikuwa wazawa wa Ketura.
5Abrahamu alimrithisha Isaka mali yake yote. 6Lakini watoto wa kiume wa masuria wake akawapa zawadi, na wakati alipokuwa bado hai, aliwapeleka katika nchi ya mashariki,#25:6 Nchi ya Mashariki: Yaani maeneo ya majangwa ya Siria na Arabia katika Mashariki na Kusini-Mashariki ya Nchi ya Palestina. Taz Amu 6:3. mbali na Isaka mwanawe.
Kifo cha Abrahamu
7Abrahamu aliishi miaka 175. 8Alifariki baada ya kuishi maisha marefu na ya fanaka, akajiunga na wazee wake#25:8 Akajiunga na wazee wake: Lugha ya Kiebrania ya mfano ambayo hutumika mara kwa mara katika A.K. labda kutokana na mila au desturi ya kuwazika waliokufa katika makaburi ya familia pamoja na watu wa jamaa waliokufa na kuzikwa hapo. Taz Mwa 23:4 maelezo. waliomtangulia. 9Isaka na Ishmaeli, wanawe Abrahamu, wakamzika baba yao katika pango la Makpela,#25:9 Makpela: Taz Mwa 23:19. mashariki ya Mamre kwenye shamba lililokuwa la Efroni, mwana wa Sohari, Mhiti. 10Abrahamu alikuwa amenunua shamba hilo kwa Wahiti. Huko ndiko alikozikwa Abrahamu na mkewe Sara. 11Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu alimbariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akawa anaishi karibu na kisima cha Beer-lahai-roi.
Wazawa wa Ishmaeli
(1 Nya 1:28-31)
12Hawa ndio wazawa wa Ishmaeli mwanawe Abrahamu ambaye Hagari Mmisri, aliyekuwa mjakazi wa Sara, alimzalia Abrahamu. 13Hii ni orodha yao kufuatana na kuzaliwa kwao: Nebayothi, mzaliwa wa kwanza, Kedari, Adbeeli, Mibsamu, 14Mishma, Duma, Masa, 15Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema. 16Hao ndio watoto wa kiume wa Ishmaeli, waliokuwa asili ya makabila kumi na mawili;#25:16 Wana wa Ishmaeli waliokuwa asili ya makabila kumi na mawili: Taz Mwa 22:20-24 maelezo. makazi na vijiji vyao vilijulikana kwa majina yao. 17Ishmaeli alikuwa na umri wa miaka 137 alipofariki, akajiunga na wazee wake waliotangulia. 18Wazawa wa Ishmaeli walikaa katika eneo lililo kati ya Hawila na Shuri, mashariki ya Misri, kuelekea Ashuru.#25:18 Ashuru: Kadiri ya mazingira ya kijiografia hapa haihusu himaya au milki ya Ashuru ila yahusu eneo lililokaliwa na wazawa wa Ashurimu wanaotajwa katika aya ya 3. Taz Mwa 25:1-6 maelezo. Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu.#25:18 Walikaa kwa utengano na wazawa wengine wa Abrahamu: Rejea Mwa 16:12.
Kuzaliwa kwa Esau na Yakobo
19Hawa ndio wazawa wa Isaka mwana wa Abrahamu. 20Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu.#25:20 Padan-aramu: Jina hili lina maana ya njia ya shamba la Aramu na huenda linatumika kutaja sehemu iliyojulikana huko Aram-naharaimu au Mesopotamia. Taz Zab 60 maelezo. Rebeka alikuwa dada yake Labani. 21Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba.#25:21 Dhana au wazo la mwanamke aliyeolewa kuwa tasa linashika nafasi yake muhimu katika historia ya mababu wa Waisraeli (rejea Mwa 16:1-16; 30:1). Kutajwa kwa wazo hilo bila shaka kunatilia mkazo kuhusika kwake Mungu katika kuzaliwa kwa wale ambao wanachukua nafasi kubwa katika ahadi ya Mungu. Taz Zab 113:9 maelezo na Luka 1:25 maelezo. 22Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka,#25:22 Watoto …wakashindana tumboni mwake Rebeka: Kisa hiki cha kushindana kwa watoto mapacha tumboni mwa mama yao ni cha pekee katika Biblia yote nacho kinaashiria uhasama utakaokuwako baadaye kati ya Yakobo na Esau (rejea Mwa 27:41-47). naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu. 23Mwenyezi-Mungu akamwambia,
“Mataifa mawili yamo tumboni mwako;
makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana.
Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine;
mkubwa atamtumikia mdogo.”#25:23 Esau na Yakobo wanatajwa hapa sio kama watu binafsi ila kama mababu wawakilishi wa mataifa mawili (Edomu na Israeli) ambayo daima yalikuwa na uhasama kati yao. Taz Oba 10 maelezo.
24Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha. 25Wa kwanza alikuwa mwekundu, mwenye nywele#25:25 Nywele: Neno la Kiebrania ambalo limetafsiriwa hapa kwa “nywele” linatamkika kwa namna inayofanana na “Seiri” ambalo ni jina lingine la Esau. Taz Mwa 36:8. mwili wote; hivyo wakamwita Esau. 26Wa pili alizaliwa akiwa amemshika Esau kisigino, hivyo wakampa jina Yakobo.#25:26 Yakobo: Jina hili linatamkika katika Kiebrania kwa namna inayofanana na neno la Kiebrania lenye maana ya “kisigino”. Rejea pia Mwa 27:36 ambapo pia kutokana na matamshi yanayofanana katika Kiebrania, jina hilo linahusishwa na neno la kitenzi katika Kiebrania lenye maana ya “kudanganya”. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati Esau na Yakobo walipozaliwa.
Esau anauza haki yake
27Watoto hao wakakua; Esau akawa mwindaji hodari, mpenda maisha ya mbugani, na Yakobo akawa mtu mtulivu, mpenda maisha ya nyumbani. 28Basi, Isaka akampenda Esau kwa sababu alipenda kula mawindo yake, lakini Rebeka akampenda Yakobo.#25:25-28 Hapa kuna namna mbili za kazi ambazo zinalinganishwa: kazi ya kuwinda na kazi ya ukulima.
29Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana. 30Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu).#25:30 Hati ya Kiebrania ina mchezo wa maneno hapa kati ya jina la Edomu na neno lenye maana ya “-ekundu”; rejea aya 25. 31Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” 32Esau akasema, “Sawa! Niko karibu kufa; haki yangu ya mzaliwa wa kwanza itanifaa nini?” 33Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Basi, Esau akamwapia na kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. 34Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na dengu kiasi. Esau akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo ndivyo Esau alivyoidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 25: BHNTLK
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993