Marko 11
11
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Lk 19:28-40; Yh 12:12-19)
1Walipokaribia Yerusalemu walifika eneo la Bethfage na Bethania lililo karibu na Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wanafunzi wake wawili, 2na kuwaagiza, “Mwende katika kijiji kilichopo ngambo yenu kule, na mara tu mtakapoingia ndani yake mtakuta mwana punda amefungwa mahali na ambaye hajawahi kupandwa na mtu yeyote. Mfungueni na kisha mumlete hapa. 3Na mtu yeyote akiwauliza, ‘Kwa nini mnafanya hivi?’ ninyi mseme, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha kwenu mara moja.’”
4Hivyo wakaondoka, nao wakamkuta mwana punda huyo amefungwa katika mtaa wa wazi karibu na mlango. Wakamfungua. 5Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu na mahali pale wakawaambia, “Je! kwa nini mnamfungua mwana punda huyo?” 6Wanafunzi wake wakawaeleza yale walioambiwa na Yesu wayaeleze, nao wakawaacha waende zao.
7Kisha wakamleta mwana punda yule kwa Yesu na wakaweka mavazi yao ya ziada juu ya mwana punda, naye akampanda na kukaa juu yake. 8Watu wengi wakatandika makoti yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kwenye mashamba yaliyo jirani. 9Wote wale waliotangulia mbele na wale waliofuata walipiga kelele kwa shangwe,
“‘Msifuni#11:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia katika mstari wa 10. Mungu!
Mungu ambariki yeye
anayekuja katika Jina la Bwana!’#Zab 118:25-26
10Mungu aubariki ufalme unaokuja,
ufalme wa Daudi baba yetu!
Msifuni Mungu juu mbinguni!”
11Ndipo Yesu aliingia Yerusalemu na kwenda hadi kwenye eneo la Hekalu akizunguka na kutazama kila kitu kilichokuwepo mahali hapo. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana, aliondoka kwenda Bethania akiwa na wanafunzi wake kumi na wawili.
Yesu Aulaani Mtini
(Mt 21:18-19)
12Siku iliyofuata, walipokuwa wakiondoka Bethania, Yesu akawa na njaa. 13Na kutokea mbali akauona mti wa mtini umefunikwa kwa matawi yake mengi, hivyo akausogelea karibu ili kuona kama atakuta tunda lolote juu yake. Lakini alipoufikia hakukuta tunda lolote isipokuwa matawi tu kwani hayakuwa majira ya mitini kuwepo katika mti. 14Akauambia mtini ule, “Mtu yeyote asile matunda kutoka kwako kamwe milele!” Na wanafunzi wake waliyasikia hayo maneno.
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-17; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)
15Walipofika Yerusalemu waliingia katika viwanja vya Hekalu. Yesu akaanza kuwafukuza nje wale waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza na kununua katika eneo la Hekalu. Akapindua meza za wabadilishaji wa fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 16Pia hakumruhusu mtu yeyote abebe kitu chochote kukatiza eneo la Hekalu. 17Yesu akaanza kuwafundisha na kuwaeleza, “Je! haikuandikwa katika Maandiko kwamba: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ambapo watu wa mataifa yote wataleta maombi yao kwangu’?#Isa 56:7 Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘mahali pa wezi kujificha.’#Yer 7:11”
18Na viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria waliyasikia haya, na hivyo wakaanza kutafuta njia ya kumuua. Kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote walikuwa wamestaajabishwa na mafundisho yake. 19Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka Yerusalemu.
Mtini na Imani, Maombi na Msamaha
(Mt 21:20-22)
20Ilipofika asubuhi Yesu na wanafunzi wake walikuwa wakitembea pamoja na wakauona ule mti wa mtini umekauka kuanzia kwenye mizizi yake. 21Petro akakumbuka yale Yesu aliyosema kwa mti huo na kumwambia, “Mwalimu, tazama! Mti ule wa mtini ulioulaani umenyauka kabisa.”
22Yesu akawajibu, “Mnapaswa kuweka imani yenu kwa Mungu. 23Nawaambia kweli: Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ukajitupe katika bahari’; kama asipokuwa na mashaka moyoni mwake, Lakini akaamini kuwa kile anachokisema kitatokea, huyo atatendewa hayo. 24Kwa sababu hiyo nawaambia chochote mtakachoomba katika sala, muamini kwamba mmekipokea na haja mliyoiomba nayo itakuwa yenu, 25Na wakati wowote mnaposimama kuomba, mkiwa na neno lolote kinyume na mtu mwingine, mmsamehe mtu huyo. Na Baba yenu aliye mbinguni naye atawasamehe ninyi dhambi zenu.” 26#11:26 Nakala zingine za awali za Kiyunani zimeongeza mstari wa 26: “Lakini kama hamtawasamehe wengine, basi Baba yenu wa Mbinguni hatawasamehe ninyi dhambi zenu.”
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mt 21:23-27; Lk 20:1-8)
27Yesu na wanafunzi wake walirudi Yerusalemu. Na walipokuwa wakitembea ndani ya viwanja vya Hekalu, viongozi wa makuhani, walimu wa Sheria na wazee walimjia Yesu 28na kumwuliza, “Kwa mamlaka gani unafanya vitu hivi? Nani alikupa mamlaka ya kuvifanya?”
29Yesu akawaambia, “Nitawauliza swali, na mkinijibu, ndipo nitawaeleza kwa mamlaka gani ninafanya vitu hivi. 30Je! ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni ama ulitoka kwa watu? Sasa mnijibu basi.”
31Walijadiliana wao kwa wao wakisema, “Tukisema ‘ulitoka mbinguni’, atasema, ‘Kwa nini basi hamumuamini?’ 32Lakini kama tukisema kuwa ubatizo wa Yohana ulitoka kwa wanadamu, watu watatukasirikia.” Viongozi waliwaogopa watu, kwani watu wote waliamini kuwa Yohana kweli alikuwa nabii.
33Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatufahamu.”
Hivyo Yesu akawaambia, “Hata mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”
Iliyochaguliwa sasa
Marko 11: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International