Marko 12
12
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mt 21:33-46; Lk 20:9-19)
1Yesu alianza kuongea nao kwa simulizi zenye mafumbo: “Mtu mmoja alipanda mizabibu shambani. Akajenga ukuta kuizunguka, akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia mizabibu na kisha alijenga mnara. Baadaye alilikodisha kwa baadhi ya wakulima na akaenda safari nchi ya mbali.
2Yalipotimia majira ya kuvuna, alimtuma mtumishi wake kwa wakulima wale, ili kukusanya sehemu yake ya matunda ya mzabibu. 3Lakini wakulima wale walimkamata mtumishi yule, wakampiga, na kumfukuza pasipo kumpa chochote. 4Kisha akamtuma mtumishi mwingine kwao. Huyu naye wakampiga kichwani na kumtendea mambo ya aibu. 5Yule mmiliki wa shamba la mzabibu akamtuma mtumishi mwingine, na wakulima wale wakamuua na yule pia. Baada ya hapo alituma wengi wengine. Wakulima wale waliwapiga baadhi yao na kuua wengine.
6Hata hivyo mwenye shamba yule bado alikuwa na mmoja wa kumtuma, mwanaye mpendwa. Alimtuma akiwa mtu wa mwisho. Akasema, ‘nina hakika watamheshimu mwanangu!’
7Lakini wakulima wale walisemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye yule mrithi. Njooni tukamuue, na urithi utakuwa wetu!’ 8Kwa hiyo wakamchukua na kumuua, kisha wakautupa mwili wake nje ya shamba la mizabibu.
9Je! Mnadhani mwenye kumiliki lile shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na kuwaua wakulima wale, na kukodisha shamba lile kwa watu wengine. 10Je! Hamjayasoma maandiko haya:
‘Jiwe ambalo wajenzi wamelikataa
limekuwa jiwe kuu la msingi.
11Hii imefanywa na Bwana
na ni ajabu kubwa kwetu kuona!’”#Zab 118:22-23
12Na viongozi wa kidini wakatafuta njia ya kumkamata Yesu, lakini waliogopa lile kundi la watu. Kwani walijua ya kwamba Yesu alikuwa ameisema simulizi ile yenye mafumbo ili kuwapinga. Kwa hiyo viongozi wa kidini wakamwacha na kuondoka.
Yesu Ajibu Swali Lenye Mtego
(Mt 22:15-22; Lk 20:20-26)
13Viongozi wa Kidini wakamtumia baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kumkamata kama akisema chochote kimakosa. 14Wale waliotumwa walifika na kumwambia, “Mwalimu tunajua, kwamba wewe ni mkweli, na tena hujali yale watu wanayoyafikiri kuhusu wewe, kwa sababu wewe hubabaishwi na wadhifa wa mtu. Lakini unafundisha ukweli wa njia ya Mungu. Tuambie ni haki kulipa kodi kwa Kaisari ama la? Je! tulipe au tusilipe?”
15Lakini Yesu aliutambua unafiki wao na akawaambia, “Kwa nini mnanijaribu hivi? Mniletee moja ya sarafu ya fedha mnazotumia ili niweze kuiangalia.” 16Hivyo wakamletea sarafu, naye akawauliza, “Je! sura hii na jina hili ni la nani?” Nao wakamwambia, “Ya Kaisari.”
17Ndipo Yesu alipowaambia, “Mpeni Kaisari vilivyo vyake, na Mungu mpeni vilivyo vyake.” Wakastaajabu sana kwa hayo.
Baadhi ya Masadukayo Wajaribu Kumtega Yesu
(Mt 22:23-33; Lk 20:27-40)
18Kisha Masadukayo wakamjia. (Hawa ni wale wanaosema hakuna ufufuo wa wafu.) Wakamwuliza, 19“Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa kaka wa mtu atafariki na kumwacha mke asiye na watoto, Basi yule kaka lazima aoe mke yule wa nduguye na kuzaa naye watoto kwa ajili ya kaka yake aliyefariki. 20Palikuwepo na ndugu wa kiume saba. Wa kwanza alioa mke, naye alikufa bila kuacha mtoto yeyote. 21Wa pili naye akamwoa yule mke wa nduguye wa kwanza aliyeachwa naye akafa bila kuacha watoto wowote. Ndugu wa tatu pia alifanya vivyo hivyo. 22Ndugu wote wale saba walimwoa yule mwanamke na wote hawakupata watoto. Mwisho wa yote, yule mwanamke pia akafariki, 23Katika ufufuo, pale wafu watakapofufuka toka katika kifo, Je! yeye atakuwa mke wa nani? Kwani wote saba walikuwa naye kama mke wao.”
24Yesu akawaambia, “Hakika hii ndiyo sababu mmekosa sana: Hamyajui Maandiko wala uwezo wa Mungu. 25Kwa kuwa wafu wanapofufuka toka katika wafu, hawaoi wala kuolewa. Badala yake wanakuwa kama malaika walioko Mbinguni. 26Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, Je! hamjasoma katika kitabu cha Musa katika sura ile ya kichaka kinachoungua? Pale ndipo Mungu alipomwambia Musa, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.’#Kut 3:6 27Yeye si Mungu wa waliokufa, bali wa wale wanaoishi. Hivyo ninyi mmekosa sana.”
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mt 22:34-40; Lk 10:25-28)
28Mwalimu wa Sheria alifika naye aliwasikia wakijadiliana. Alipoona jinsi Yesu alivyowajibu vizuri sana, alimwuliza, “Je! amri ipi ni muhimu sana kuliko zote?”
29Yesu akajibu, “Muhimu sana ni hii: ‘Sikiliza, Israeli, Bwana Mungu wetu ni mmoja. 30Nawe unapaswa kumpenda Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa nafsi yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’#Kum 6:4-5 31Amri ya pili ni hii: ‘Mpende jirani yako#12:31 jirani yako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji. kama unavyojipenda mwenyewe.’#Law 19:18 Hakuna amri nyingine kubwa kuliko hizi.”
32Na mwalimu wa Sheria akamwambia, “Umejibu vema kabisa mwalimu. Upo sahihi kusema kuwa Mungu ni mmoja, na hakuna mwingine ila yeye. 33Ni muhimu zaidi kumpenda Mungu kwa moyo wako wote, kwa ufahamu wako wote, na kwa nguvu zako zote, na kumpenda jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe kuliko sadaka zote za kuteketezwa na matoleo tunayompa Mungu.”
34Yesu alipoona kwamba yule mtu amejibu kwa busara, alimwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Baada ya hapo hakuwepo mtu mwingine aliyediriki kumwuliza maswali mengine zaidi.
Je! Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mt 22:41-46; Lk 20:41-44)
35Yesu alipokuwa akifundisha katika mabaraza ya Hekalu, alisema, “Inawezekana vipi walimu wa Sheria kusema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36Daudi mwenyewe kwa kupitia Roho Mtakatifu alisema,
‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
nami nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’#12:36 chini ya udhibiti wako Mafundisho ya Yesu katika Lk 10:25-37 yanaonesha kwa uwazi kuwa hii ni pamoja na yeyote mwenye uhitaji. #Zab 110:1
37Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Itakuwaje tena Kristo awe yote Bwana na pia mwana wa Daudi?”
Hapo lilikuwepo kundi kubwa la watu liliokuwa likimsikiliza kwa furaha.
Yesu Anawakosoa Walimu wa Sheria
(Mt 23:6-7; Lk 11:43; 20:45-47)
38Katika mafundisho yake alisema, “Jihadharini na walimu wa Sheria.” Wao wanapenda kutembea huko na huko katika mavazi yanayopendeza huku wakipenda kusalimiwa masokoni, 39Hao wanapenda kukaa viti vya mbele katika masinagogi na kupewa sehemu muhimu zaidi za kukaa katika karamu za chakula. 40Hawa huwadanganya wajane ili wazichukue nyumba zao na wanasali sala ndefu ili kujionesha kwa watu. Watu hawa watapata hukumu iliyo kubwa zaidi.
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Lk 21:1-4)
41Yesu aliketi mahali kuvuka pale palipokuwepo na sanduku la matoleo, alitazama jinsi ambavyo watu walikuwa wakiweka sadaka zao sandukuni. Matajiri wengi waliweka fedha nyingi. 42Kisha mjane maskini alikuja na kuweka sarafu mbili ndogo za shaba, ambazo zilikuwa na thamani ndogo sana.
43Yesu aliwaita wanafunzi wake pamoja na kuwaambia, “Nawaambieni ukweli mjane huyu maskini ameweka sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kwamba ametoa zaidi ya matajiri wote wale.” 44Kwa kuwa wote walitoa kile cha ziada walichokuwa nacho. Lakini yeye katika umasikini wake, aliweka yote aliyokuwa nayo. Na hiyo ilikuwa fedha yote aliyokuwa nayo kutumia wa maisha yake.
Iliyochaguliwa sasa
Marko 12: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International