Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 7

7
Hotuba ya Stefano kwa Baraza
1Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”
2Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani, 3akamwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na katika jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha.’#7:3 Mwanzo 12:1
4“Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa. 5Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Ibrahimu hakuwa na mtoto. 6Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’ 7Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’#7:7 Mwanzo 15:13, 14 8Ndipo akampa Ibrahimu agano la tohara. Naye Ibrahimu akamzaa Isaka na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaka akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale baba zetu wa zamani kumi na wawili.
9“Kwa sababu hao baba zetu wa zamani walimwonea wivu Yusufu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye. 10Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata. Tena Mungu akampa Yusufu kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Naye Farao akamweka kuwa mtawala wa Misri na wa jumba lote la kifalme.
11“Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula. 12Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza. 13Walipoenda mara ya pili, Yusufu alijitambulisha kwa ndugu zake; naye Farao akapata habari kuhusu ndugu za Yusufu. 14Ndipo Yusufu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote; kwa jumla walikuwa watu sabini na watano. 15Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia. 16Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Ibrahimu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
17“Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Ibrahimu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri. 18Ndipo ‘mfalme mwingine ambaye hakufahamu habari za Yusufu akatawala Misri’#7:18 Kutoka 1:8. 19Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.
20“Wakati huo Musa alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani mwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu. 21Walipomweka nje mtoni, binti Farao akamchukua akamlea kama mtoto wake. 22Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.
23“Musa alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli. 24Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi. 25Musa alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa. 26Siku iliyofuata Musa aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’
27“Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Musa kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? 28Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’#7:28 Kutoka 2:14 29Musa aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.
30“Baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Musa jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 31Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Mwenyezi Mungu, ikisema: 32‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’#7:32 Kutoka 3:6 Musa alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.
33“Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu. 34Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’#7:34 Kutoka 3:5, 7, 8, 10
35“Huyu ndiye Musa waliyemkataa waliposema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kupitia kwa yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. 36Aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu#7:36 yaani Bahari ya Mafunjo, na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.
37“Huyu ndiye yule Musa aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe.’#7:37 Kumbukumbu 18:15 38Huyu ndiye yule Musa aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.
39“Lakini baba zetu walikataa kumtii Musa, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena. 40Wakamwambia Haruni, ‘Tufanyie miungu itakayotuongoza, kwa maana mtu huyu Musa aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’#7:40 Kutoka 32:1 41Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42Ndipo Mungu akageuka, akawaachia waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii:
“ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka
kwa miaka arobaini kule jangwani,
ee nyumba ya Israeli?
43La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki,
na nyota ya mungu wenu Refani,
vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu.
Kwa hiyo nitawapeleka mbali’#7:43 Amosi 5:25-27 kuliko Babeli.
44“Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani, ambalo lilitengenezwa kama Mungu alivyomwelekeza Musa, kulingana na kielelezo alichokiona. 45Baada ya kupokea Hema, baba zetu waliingia nalo walipokuja na Yoshua wakati walimiliki nchi, Mungu alipoyafukuza mataifa mbele yao. Nalo lilidumu katika nchi hadi wakati wa Daudi, 46ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. 47Lakini Sulemani ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
48“Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:
49“ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi,
nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.
Mtanijengea nyumba ya namna gani?
asema Mwenyezi Mungu.
Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?
50Je, mkono wangu haukuumba vitu hivi vyote?’#7:50 Isaya 66:1, 2
51“Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho wa Mungu, kama walivyofanya baba zenu. 52Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji. 53Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”
Stefano apigwa mawe
54Wazee wa Baraza la Wayahudi#7:54 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno. 55Lakini Stefano, akiwa amejawa na Roho wa Mungu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Isa akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”
57Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58Wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
59Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Isa, pokea roho yangu.” 60Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana, usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 7: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia